Gladness Mallya BAADA ya kutokea vifo vya mahujaji zaidi ya mia saba waliokuwa wakishiriki Hija karibu na mji mtakatifu wa Waislam wa Makka, staa wa filamu za Kibongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto au King Majuto’ amesimulia alivyonusurika kwenye tukio hilo la kukanyagana.
Prof. Ibrahim Lipumba na baadhi ya mahujaji.
Akizungumza na gazeti hili mke wa Mzee Majuto, Aisha alisema baada ya kupata taarifa za mahujaji kufariki na mumewe alikuwa kwenye msafara huo alishtuka mno ambapo haraka alifanya mawasiliano naye na kumwelezea kwamba alinusurika na tukio hilo la kusikitisha.
Wahanga wa maafa ya mkanyagano kwenye hija mjini Makka, Saudi Arabia
“Nimeongea na Mzee Majuto kasema yuko vizuri na alinusurika kwenye mkanyagano huo kwani mahujaji walikuwa ni wengi sana ambapo walikuwa wakienda sehemu maalum kwa ajili ya kumpiga mawe shetani hivyo wakashindwa kupishana na kusababisha mkanyagano huo.
“Anasema alishuhudia watu walivyokuwa wakikanyagana ambapo wengine walijeruhiwa vibaya na vifo vikiwa ni vingi lakini anamshukuru Mungu amenusurika na tukio hilo baya na la kihistoria maishani mwake,” alisema Aisha.
Aliendelea kusema japokuwa mumewe amemhakikishia kwamba yuko salama lakini bado ana hofu kubwa mpaka sasa na kikubwa wanaendelea kumuombea kwa Mungu ili aweze kurudi salama.
“Yaani mpaka sasa tuna hofu kubwa mno, tunamuomba Mwenyezi Mungu amrudishe salama pia kwa mahujaji waliofariki tunamuomba Mwenyezi Mungu awaweke mahali pema peponi na ndugu zao tunawaombea faraja katika kipindi hiki kigumu,” alisema Aisha.
Mzee Majuto alikuwa ni miongoni mwa mahujaji waliokwenda Makka kwa ajili ya kuhiji ambapo mpaka Jumamosi vifo vya mahujaji vilikuwa vimefikia zaidi ya mia saba wakiwemo Watanzania watano.
Post a Comment