WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maafisa watano na watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.
Akizungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari pamoja na viongozi wa TRA katika ziara ya kushtukiza leo mchana (Ijumaa, Novemba 27, 2015), Waziri Mkuu amewataka Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Rished Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Lusekelo Mwaseba wahahakikishe wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na kwamba fedha hizo zinapatikana na zinarudi Serikalini.
Akitangaza uamuzi huo baada ya kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Serikali bandarini hapo, Waziri Mkuu aliwataja maafisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Bw. Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Bw. Habibu Mponezya.
“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,” alisema Waziri Mkuu.
Maafisa wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa kitengo cha TEHAMA, Bw. Haruni Mpande, Bw. Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani), na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Bw. Eliachi Mrema. “Hawa wanasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na pia wawe mikononi mwa polisi,” alisema.
Pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani. Watumishi hao ni Bw. Anangisye Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw. Robert Nyoni.
Post a Comment