Featured

    Featured Posts

WANASIASA. HAWA WATAJWA KUHUSIKA NA MAUAJI YA ALBINO KUELEKEA UCHAGUZI 2015

Wanasiasa wamenyooshewa vidole, wakihusishwa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi baada ya matukio hayo kuhusishwa na harakati za kuelekea katika uchaguzi mkuu.Vyama vya watu wenye ulemavu pamoja na baadhi ya wadau kutoka vyama vya siasa, vimetaka Serikali kutopuuzia dhana hiyo ya kuhusisha harakati za kisiasa na mauaji hayo.
 Aidha, Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania, kimesema kiko katika maandalizi ya kufanya maandamano ya amani hadi Ikulu kwa ajili ya kumwona Rais Jakaya Kikwete wapange mikakati ya kutokomeza mauaji hayo ya ukatili .

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Walemavu na Vyama vya Siasa nchini, mwanachama kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Abdallah alisema katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi, alisema albino wanaishi kwa wasiwasi kutokana na uwezekano wa mauaji hayo kuanza kuibuka tena kwa kasi.
“Mimi mwenyewe nina tatizo la ngozi (albino), hivi sasa tuko kwenye kipindi cha uchaguzi, na tetesi ni kwamba wengi wanauawa kwa imani potofu za baadhi ya watu kutaka madaraka, tusaidieni jamani ukweli ni kwamba tunaishi kwa hofu,” alisema.
Alisema ni vyema Serikali ikaacha kupuuzia tetesi hizo za kuwahusisha baadhi ya watu wanaotaka madaraka na kuagiza watu wenye ulemavu wauawe kwa imani za kishirikina.
Alitaka hatua madhubuti zichukuliwe kuokoa maisha ya Watanzania hao.
“Jamani tujue kuwa hii ni damu inayomwagika ni ya ndugu zetu, kama hatua zisipochukuliwa inaweza kuwa laana kwa vizazi vyetu. Tukijipanga Tanzania tunaweza kuwa salama,” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP), Said Soud alisema jamii inatakiwa kutambua kuwa ni dhambi watu kufikiria kuwa wanaweza kupata utajiri na madaraka kupitia mauaji au viungo vya watu wenye ulemavu.
“Hili naomba likemewe kwa nguvu zote, hii ni dhambi kubwa, sisi wanasiasa tutumie majukwaa kukemea dhambi hii, lakini pia Serikali nayo itekeleze kwa vitendo sheria zilizopo na kuwaadhibu vikali wale wote wanaohusika na dhambi hii,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania, Ernest Kimaya kwa upande wake alisema, kwa sasa tatizo hilo linazidi kuwa sugu.
Alisema tangu mauaji hayo yaanze mwaka 2006, hadi juzi alipouawa Yohana Bahati, maalbino 76 wameuawa kikatili na watu wasiojulikana.
Ushirikina
Hivi karibuni, katika semina iliyoandaliwa na Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), baadhi ya washiriki walitaja uchaguzi mkuu kuchochea ongezeko la mauaji ya wenye ulemavu kutokana na wagombea kutumia mbinu chafu na dhaifu.
Katika semina hiyo iliyofadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika lake la Kimataifa la Maendeleo na Misaada (Sida), ilielezwa na baadhi ya wachangiaji kwamba, ongezeko la mauaji ya albino katika kipindi cha uchaguzi, linatokana na imani potofu miongoni mwa wanasiasa uchwara.
Miongoni mwa wachangiaji katika semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Diwani wa Kata ya Sunya, wilayani Kiteto, Manyara, Mussa Brighton (CCM) aliyeomba serikali kutafuta mbinu za kudumu za kukabili wanasiasa wa aina hiyo.
Juzi, Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja huo (UNDP), Alvaro Rodriguez katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, pia aligusia kuwapo taarifa zinazohusisha wanasiasa na mauaji hayo.
Alisema mashambulio dhidi ya watu wenye albinism, yanaelezwa kuwa yanasababishwa na imani za kishirikina na kwamba kutoka mwaka 2000 hadi sasa, watu 74 wenye ulemavu huo wameuawa.
Maandamano

“Kutokana na tatizo hili kuzidi kuwa sugu chama chetu kimeanza maandalizi ya maandamano ya amani na kupeleka kilio chetu kwa Rais ili tuweze kushauriana utaratibu wa kupata suluhu ya kudumu ya tatizo hili,” alisema Kimaya.

Alisema katika maandamano hayo watayafanya Machi 2, mwaka huu na kwamba, pamoja na kupeleka kilio hicho kwa Rais, pia watafanya sala maalumu kwa ajili ya wote waliopoteza maisha yao kwa kuuawa kikatili
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Total Pageviews

Copyright © DAILY MAIL | Designed By Code Nirvana