JUZI Watanzania tulipata pigo la kumpoteza Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba. Alikuwa ni msanii nyota na mwakilishi wa watu wa Mbinga na kubwa alitetea maslahi ya Watanzania akiwa bungeni.
Taarifa za msiba huo zilienea kwa kasi kwenye mitandao hiyo na kufanya watu wengi kufikiwa na taarifa hizo za kuhuzunisha.
Pamoja na kupeana taarifa hizo za kusikitisha, baadhi ya watu ama kwa ulimbukeni wa mitandao, ama kwa kutojali heshima ya marehemu, tangu kupatikana kwa taarifa za kifo chake cha ghafla wamekuwa wakisambaza picha ya mwili wa marehemu.
Huku katika mazingira ya kawaida ni kukosa maadili, kushindwa kujiheshimu na pia kukosa ustaarabu wa kuheshimu na kusitiri binadamu aliyeondoka duniani.
Picha hiyo iliyokuwa imetumwa kwenye makundi ya marafiki kwenye mitandao ya kijamii, ilinifanya kuumia zaidi, kwani waliopata taarifa hiyo iliyoambatana na mwili wa marehemu ukiwa umelala kwenye kitanda katika hali ile sidhani kama walikuwa ni watu stahiki, sembuse kuwa na uwezo wa kuiondoa akilini.
Ninavyoona haikuwa sahihi kuiweka picha ya marehemu, watoa taarifa wangeweza hata kutumia picha ya kiongozi huyo akiwa kwenye moja ya shughuli zake wakati wa uhai wake ambazo ziko nyingi kwenye mitandao kuliko ile.
Tukio hilo lilinikumbusha matukio mengi na picha nyingi ambazo watu wamekuwa wakizituma bila kujua kuwa zitaleta ukakasi kwa wale wanaotumiwa, kama vile picha za ajali, au ile iliyomuonesha mwanamke aliyeunguzwa na mumewe sehemu za siri au mtoto albino alivyocharangwa mapanga na nyingine nyingi ambazo naamini hazifuati maadili katika kupashana habari wala faragha ya mtu.
Ukiangalia kwa undani picha hizi za kiongozi wetu huyo, zinaonesha kabisa kuwa zimepigwa na watu waliokuwapo karibu na marehemu wakati huo na hawa pasi shaka ni wauguzi au madaktari au wahudumu, katika hali ya kawaida hakuna ndugu ambaye atapigapicha kisha aiweke kwenye mitandao.
Jambo la kujiuliza kama waliofanya hivyo ni kati ya madaktari na wauguzi, maadili ya kazi yao yako wapi. Wote tunajua kuwa siri ya mgonjwa au marehemu anayefika katika hospitali zetu ziko kwenye mikono ya watoa huduma hao, sasa iweje pia hiyo isambae kwenye mitandao? Hii inasikitisha sana kwani huu ni uvunjaji wa maadili ya kazi yao.
Nakumbuka, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilianzisha kampeni ya Futa Delete Kabisa ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza matumizi mabaya ya mitandao ingawa bado kuna watu chache ambao bado wanafanya hivyo.
Ikumbukwe kuwa maendeleo ya teknolojia yana manufaa makubwa kwa wale wanaotaka kutumia kwa ajili ya manufaa na kupewa taarifa za kuwafanya wapige hatua za maendeleo, lakini pia zina ubaya wake kwa watu ambao hawataki kutumia kwa maendeleo.
Hao walioanza kutumia maendeleo ya mitandao kamwe huwezi kuona picha na maiti zikiwa zinaoneshwa ovyo, mfano mzuri ni kifo cha Michael Jackson, hakuna mtu anayeweza kutafuta hiyo pia, sasa kwa nini iwe kwetu?
Kufanya hivyo ni dalili ya ulimbukeni wa watumiaji wa teknolojia hii.
Pamoja na jeshi la Polisi kuwa na jukumu la kupambana na wahalifu wa mitandao, ikiwa ni pamoja na wanaotumiwa kusambaza taarifa za chuki, kashfa kwa watu wengine na hata picha zinazokwenda kinyume na maadili ya watanzania, kazi hii inatakiwa jamii nzima ishirikiane kutokomeza.
Jambo la kwanza kwa jamii ni kuhakikisha unawaambia washirika katika makundi ya kijamii, kutotuma picha za ajabu, au taarifa zisizo za maana au zenye kueneza chuki, pili tunaweza kukubaliana kuwaondoa wale wanaokiuka maadili na tatu kutokuwa mmoja wa watu wanaosambaza vitu kama hivyo.
Hivyo, Watanzania wakati umefika sasa, kushirikiana katika kukataa hili la udhalilishaji na kuwa chombo cha kusambaza mambo yasiyo na msingi, na badala yake tutumie mitandao katika kutafuta taarifa za kujenga na kuweza kutuletea maendeleo.
Post a Comment